Dalili Za Uti
UTI, yaani Urinary Tract Infections, ni magonjwa au maambukizi katika njia ya mkojo. Maambukizi hayo huletewa na vimelea (bakteria) au kitu chochote kinachoweza kusababisha shida katika njia ya mkojo.
Vitu hivi vinaweza kuingia kwenye njia ya mkojo kutoka nje au ndani ya mwili. Maambukizi haya hayabagui jinsia wala umri, kwani yanaweza kumpata yeyote.

UTI usipotibiwa, unaweza kuenea na kuadhiri viungo vingine vinavyoshikana na njia hii kama vile kibofu cha mkojo (bladder), mirija inayoshikanisha kibofu cha mkojo na figo (ureter) na sehemu inayotoa mkojo kutoka kwenye kibofu na kuutoa nje (urethra). Kwa ufupi, UTI huadhiri viungo ambavyo hupitisha mkojo kutoka mwilini na kuutupa nje.
Wanawake huadhirika zaidi na UTI ikilinganishwa na wanaume. Hii ni kwasababu za kimaumbile. Maambukizi haya huweza kusababishwa na historia ya familia au kufanya mapenzi na watu kadhaa bila kutumia kinga.
Wasichana wadogo walio chini ya umri wa miaka miwili na wavulana ambao hawajatahiriwa pia huupata ugonjwa huu mara zaidi.
Vimelea vinavyosababisha UTI ni kama vile Staphylococcus saprophyticus na Escherichia coli (E Coli). Asimilia chache ya maambukizi haya huweza kuletwa na virusi au fangasi (fungus).
Dalili za UTI
Dalili za UTI ambazo mtu hupata hulingana na sehemu ambayo imeathirika. Hivyo basi, dalili zitakua tofauti wakati mrija wa mkojo, kibofu au figo zimeathirika. Dalili hizo zimeelezwa kwa kina hapa.
Dalili iwapo mrija wa kutoa mkojo kwenye kibofu umeathirika
- Mtu huhisi kama kwamba anachomeka wakati anapokojoa. Kuchomeka huko huweza kuzidi na kuwa uchungu (maumivu).
- Shida wakati wa kukojoa kama vile kushindwa kudhibiti kasi ya mkojo.
- Mtu anaweza kukawia sana kabla ya mkojo kutoka.
- Mtu kuhisi kukazwa sana lakini aendapo chooni, mkojo kidogo tu ndio hutoka.
- Kukojoa kiasi kidogo cha mkojo mara nyingi.
Dalili za UTI iwapo kibofu cha mkojo kimeathirika
- Mtu huweza kuona damu kwenye mkojo anapoenda haja. Hii huweza ikawa dalili ya UTi ingawaje magonjwa mengine pia huleta dalili sawa na hii.
- Pia mtu huweza kuhisi maumivu kwenye nyonga (hip area). Hii huathiri wanawake zaidi.
- Kuhisi kama kibofu kimejaa wakati wote.
- Dalili ingine ni kuwa na maumivu chini ya kitovu.
- Dalili ya mwisho ni mtu kukujoa mara kwa mara na kuhisi uchungu anapokojoa.
Dalili iwapo figo zimeathirika
- Mtu hupata kichefuchefu mara kwa mara iwapo ugonjwa wa UTI umemwathiri. Kichefuchefu ni hali ya kuhisi kutapika.
- Maumivu kwenye mbavu.
- Dalili hii ya kichefuchefu huweza kuzidi na mwathiriwa kuanza kutapika anapokula chakula.
- Dalili ingine ni mtu kuumwa na upande wa juu wa mgongo. Hii inaweza kuwa kuanzia katikati ua uti wa mgongo, kwenye mabega na kwenye shingo.
- Dalili hizi huweza kuambatana na homa kali.
- Dalili ya mwisho ni mtu kuhisi baridi kali na kutetemeka sana pasi na kuwepo kwa baridi.
Kuna dalili za UTI ambazo hutokea wakati ugonjwa huu umeathiri mahali popote kwenye njia hii ya kutoa mkojo. Nazo ni kama rangi ya mkojo kugeuka na kuwa mawingu mawingu, pia unaweza ukawa rangi ya brauni au pinki.
Maradhi yanapozidi, mkojo huwa na rangi nyekundu na wenye harufu kali. Wanaume huweza kupata maumivu wakati wa kwenda haja kubwa.
Hatari za UTI
Magonjwa yanayosababisha UTI ni rahisi kutibiwa kutumia dawa za antibaotiki. Hata hivyo, mtu huhimizwa kupata matibabu mara moja na kumaliza dawa kama alivyoagizwa na daktari. Maradhi haya yasipotibiwa huweza kuleta shida zaidi kama vile:
- Maradhi kujirudia baada ya kutibiwa na kupona kabisa. Hii hutokea sana sana kwa wanawake ambao wanaathirika na UTI zaidi ya mara tatu.
- Kuharibika kwa figo kutokana na shida zinazotokea kama vile kidney infection (Pyelonephritis). Hii huweza kutokea mtu asipopokea matibabu.
- Wanawake huweza kuwazaa watoto mapema (premature birth) au kuzaa watoto wenye uzani mdogo zaidi.
- Njia ya mkojo (urethra) kwa wanaume hufinyika na kuwa ndogo. Hii hutokana na ugonjwa wa Urethritis kutokea mara kadhaa. Pia maradhi kama gonococcal urethritis huweza kusababisha shida hii.
- Mwisho, ugonjwa wa UTI unapofika kwenye figo kupitia mshipa wa kutolea mkojo, mtu huweza kupata Sepsis. Hii ni shida inayokumba figo na kuziangamiza kabisa. Hii ni mojawapo ya shida hatari kabisa kwani inaweza kumfanya mwathiriwa kuaga.
Hali zinazochangia kupata maradhi ya UTI
- Maumbile: Wanawake huwa na njia fupi ya kutoa mkojo (urethra) kuliko wanaume. Hivyo basi, vimelea na vitu vinavyosababisha UTI huweza kuingia kwenye njia ya mkojo haraka.
- Ngono: Watu wanaofanya mapenzi huambukizwa UTI zaidi ya wasiofanya mapenzi kama vile watoto. Walio na wapenzi wengi huwa hatarini ya maambukizi zaidi.
- Njia za kupanga uzazi: Wanawake wanotumia njia za diaphragm kupanga uzazi hupata maambukizi zaidi ya wanaotumia kinga aina ya spermicidals.
- Kufunga uzazi: Wanawake waliofikisha miaka ya kufunga uzazi huwa hatarini zaidi kutokana na upungufu wa estrogen.
- Kukosa kinga mwilini: Mtu anapokua na maradhi yanayopunguza kinga ya mwili kama vile ugonjwa wa sukari au Ukimwi, anaweza kuupata ugonjwa huu kwa urahisi.
- Upasuaji: Iwapo mtu amefanyiwa upasuaji karibu na njia ya mkojo, inaongeza uwezekano wake wa kupata UTI.
- Kufungika kwa mishipa ya figo: Mawe yanayokuwa kwenye figo huleta shida za kufungika kwa mishipa ya kutoa mkojo kwenye figo. Hii huweza kuongeza uwezekano wa maradhi ya UTI.
- Shida za njia ya mkojo: Watoto wengine huzaliwa wakiwa na shida kwenye njia zao za mkojo. Kwa mfano hawawezi kudhibiti mkojo au wanatumia vifaa vinavyowasaidia kutupa mkojo nje. Hii ni njia inayoongeza hatari ya kupata UTI.
Matibabu
UTI hutibiwa kwa dawa za antibaotiki. Hata hivyo vimelea vya UTI huweza kuzoea dawa na kutopona. Hii hutokea sana sana mtu anapopata ugonjwa huu zaidi ya mara tatu kwa mwaka.
Hii inapofanyika, daktari huweza kumpangia mtu njia spesheli za kupambana na UTI. Njia hizo za matibabu ni:
- Kunywa dawa za antibaotiki kwa kiasi kidogo kwa muda mrefu. Hii huzuia kuchipuka tena kwa maradhi ya UTI.
- Kunywa dosi moja ya antibaotiki mara tu mtu anapofanya mapenzi. Ngono ni njia inayoongeza kutokea kwa maradhi haya.
- Kunywa antibaotiki kwa siku moja au mbili dalili zinapoanza kujitokeza.
- Kutumia bidhaa za kujipima nyumbani na kujua iwapo maradhi yamo au yanaanza kutokea
Hitimisho
Dalili za UTI ambazo zimetajwa hapa ni baadhi ya zile ambazo huhusishwa sana na maradhi ya UTI. Hata hivyo, ugonjwa huu ni mgumu kujua iwapo upo bila kupimwa na daktari.
Hivyo basi, maandishi haya yanafaa kusaidia mtu kuuelewa ugonjwa wa UTI tu. Mtu anapoona kuwa ana dalili hizi, anahimizwa kufika kituoni cha afya ili kutibiwa mapema.
Utafiti
- http://www.webmd.com/women/guide/your-guide-urinary-tract-infections?page=2
- http://www.mayoclinic.org/diseases-conditions/urinary-tract-infection/basics/risk-factors/con-20037892
- http://www.nhs.uk/Conditions/Urinary-tract-infection-adults/Pages/Introduction.aspx
- http://www.nhs.uk/Conditions/Urinary-tract-infection-adults/Pages/Introduction.aspx
- http://www.healthline.com/health/bladder-infection
- http://www.medicinenet.com/urinary_tract_infection/article.htm